Kilimanjaro Stars mikononi mwa Zanzibar Heroes leo

Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes zinachuana leo kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili kombe la Chalenji nchini Kenya.

Katika michezo yao ya mzunguuko wa kwanza, Kilimanjaro Stars ililazimishwa suluhu ya 0-0 na Libya wakati Zanzibar Heroes iliilaza Rwanda mabao 3-1.

Ni mchezo ambao Kilimanjaro Stars itahitaji ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Katika mchezo huo Kilimanjaro Stars itamkosa Mbaraka Yusuph kutokana na kusumbuliwa na mejeraha ya misuli.

Hata hivyo kocha Ninje amesema ana washambuliaji wanne ambao atawatumia kuziba nafasi hiyo ya Mbaraka.

Nahodha Himid Mao amesema mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wako tayari kupambana kupata matokeo ya ushindi kwakuwa kila mmoja wao ana morali kubwa na nia ya kupata ushindi.

Amesema kikubwa watatakiwa kutulia na akili zao kuzielekeza uwanjani kuhakikisha Kilimanajro Stars inabeba pointi zote 3.

Kwa upande wake Morocco amesema hana wasiwasi Kilimanjaro Stars ni timu ambayo anaifahamu vizuri na wachezaji wanafahamiana pia.

Morocco amesema anatarajia ushindi wa pili mfululizo leo na kujiweka katika mazingira mazuri ya kwenda Nusu Fainali ya michuano hiyo.