Utata tuta la Chirwa

Waamuzi wakongwe wa soka nchini wamemkosoa mwamuzi wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya URA kwa kutoamuru penati ya Chirwa irudiwe.

Miongoni mwa waliotoa maoni yao ni Katibu wa Kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye pia ni mwamuzi mstaafu, Kenedy Mapunda.

Mapunda anasema kisheria penalti ya Chirwa ilipaswa kurudiwa kutokana na golikipa huyo kutoka kwenye mstari wa goli kwa hatua mbili mbele kabla ya kupigwa kwa mpira.

"Kosa la kwanza ni kitendo cha golikipa kutoka mbele kabla ya mpira kupigwa, lakini pia mwamuzi alipaswa kuamuru penalti ile kurudiwa kwa mujibu wa kanuni," alisema Mapunda.

Kauli ya Mapunda pia iliungwa mkono na mwamuzi mstaafu, Omari Abdulkadir, ambaye alisema waamuzi wa mechi ya URA dhidi ya Yanga hawakutenda haki kwenye penalti ya Chirwa.

"Golikipa anaruhusiwa kusogea akiwa kwenye mstari wake kwenda kushoto au kulia lakini haruhusiwi kusogea kwenda mbele," Abdulkadir alisema na kuongeza kuwa:

“Sheria inaweka wazi. Kitendo kama kile mwamuzi alitakiwa kutoa uamuzi wa penalti irudiwe kama mpigaji alikosa, lakini kama lingeingia goli, goli lingekubalika.

"Niliuangalia mpira na kitendo kile nilikiona, nilifikiri penalti ingerudiwa... unajua golikipa siyo asikie filimbi ndiyo atoke kwenye mstari wake, hapana hata kama filimbi imepigwa anatakiwa asitoke kwenye mstari wa goli mpaka mpira upigwe."

Yanga iliondoshwa katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi kwa mikwaju 5-4 ya penati, Obrey Chirwa akikosa penati ya Yanga.