Simba yampelekea Niyonzima India kutibiwa

Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba, Haruna Niyonzima ambaye amekuwa nje kwa wiki kadhaa kutokana na majeruhi, anatarajiwa kuondoka nchini kesho Jumatano kuelekea India kwa matibabu ya goti.

Niyonzima alijiunga na Simba akitokea klabu ya Yanga, ameichezea timu hiyo mechi chache za ligi kabla ya kukaa pembeni kutokana na maumivu ya goti.

Mchezaji huyo ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) amesaini mkataba wa miaka miwili na Simba.

Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim “Try Again” Abdallah alisema kuwa maandalizi ya safari ya mchezaji huyo yamekamilika na lengo lao kubwa ni kuona anapona na kuitumikia klabu yake.

Abdallah alisema kuwa mipango ya awali ilikuwa mchezaji huyo aondoke leo, lakini kutokana na sababu mbalimbali waliamua kuisogeza safari hiyo mpaka kesho Jumatano.

“Ni jukumu letu kumtibia mchezaji, siyo Niyonzima tu, hata Saidi Mohamed naye alikwenda kutibiwa India na kurejea, japo hajaanza kuitumikia timu kwa kudaka golini, lakini anaendelea vizuri na tunatarajia ataanza kuitumikia klabu kama wachezaji wengine,” alisema Salim.

Alisema kuwa wapo makini kwa upande wa afya za wachezaji na ndiyo maana walimzuia Niyonzima kufanya mazoezi ili kuangalia maendeleo ya maumivu ya goti mpaka kufikia sasa anatakiwa kutibiwa nje ya nchi.

Salim alisema kuwa wameweka malengo makubwa kwa timu yao na wanashukuru kwa sasa wanaenda vizuri kutokana na rekodi ya kutofungwa na kuongoza ligi kwa idadi kubwa ya pointi.

“Niyonzima yupo nje ya uwanja na timu inafanya vizuri, hii imetokana na kazi nzuri ya usajili, tuna timu yenye wachezaji wengi wazuri, wanajituma na ndiyo siri ya mafanikio mpaka sasa,” alisema.