Nyoso afungiwa mechi tano

Kamati ya nidhamu ya TFF imemfungia beki wa Kagera Sugar Juma Nyoso kucheza mechi tano pamoja na faini yashilingi Tsh. 1,000,000 (Milioni moja) kwa kosa la kumpiga shabiki baada ya mchezo wa VPL kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Afisa Habari wa TFF Clifford Ndimbo amesema Kamati ya Nidhamu ya TFF ilijadili shauri la Nyoso ambalo lilifikishwa kwenye kamati hiyo baada ya kupokea taarifa ya mchezo.

“Juma Nyoso alituhumiwa kumpiga shabiki baada ya kumalizika kwa mchezo kinyume na kanuni za ligi kuu zinazozungumzia mchezo wa kiungwana.”

“Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mchezo ambayo imeeleza tukio la kupishana kwa Juma Nyoso na shabiki ambaye alikuwa amebeba vuvuzela na Juma Nyoso akaonekana kusimama na kuanza kumpiga shabiki yule kwa kutumia kiatu na baadaye akamuinamisha na kuanza kumpiga kwa kutumia goti.”

“Kamati ilimwita Nyoso kujitetea, kwa upande wake alikataa madai hayo ya kumpiga shabiki. Alisema alichofanya ilikuwa ni kumkunja tu shabiki huyo lakini hakumpiga.”

“Kamati imemtia hatiani Juma Nyoso kupitia kanuni za ligi kuu na katiba ya TFF lakini ilipokea taarifa za nyuma za Nyoso kwamba aliwahi kuadhibiwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu. Kwa hiyo kamati imemfungia Nyoso mechi tano pamoja na faini ya shilingi 1,000,000 (milioni moja).”