Pluijm aipania Yanga kombe la FA

Baada ya timu yake kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Kocha Mkuu wa Singida United, Hans van der Pluijm, amesema anazielekeza nguvu zake katika mechi ya hatua ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Yanga.

Kikosi hicho cha Pluijm juzi kilijiondoa kabisa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana ikiwa nyumbani na Ndanda FC kutoka Mtwara.

Singida United imetinga robo fainali ya kombe la FA baada ya kuifunga Polisi Tanzania kwenye mchezo wa hatua ya 16 Bora na itaikaribisha Yanga kati ya Machi 31 na Aprili Mosi mkoani Singida.

Pluijm amesema mashindano ya Kombe la FA ndiyo pekee ambayo wanaweza kuwapa kombe la kwanza msimu huu baada ya kufanya vibaya kwenye Kombe la Mapinduzi na Ligi Kuu Bara ambayo inaelekea ukingoni.

Pluijm alisema kwamba atakiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha hawarudii makosa ambayo wameyafanya kwenye mechi za Ligi Kuu huku akisema nyota wake wameiva tofauti na walivyokutana na Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

"Ili ushiriki mashindano ya CAF ni ama uwe bingwa wa Ligi Kuu au Kombe la FA, sisi tumebakiza nafasi hii moja kwa hiyo tunahitaji kushindana na kuipata, tumepata sare nyingi sana kwenye ligi ambazo zimetuumiza na kututoa kwenye mbio za ubingwa, naijua Yanga na wachezaji wangu wanaijua pia," alisema Pluijm.

Ubingwa wa FA uko wazi baada ya Simba iliyokuwa inaushikilia kutolewa katika mashindano hayo na timu ya daraja la pili ya Green Warriors ya Mwenge Dar es Salaam.