Msuva mwendo mdundo Morocco, atupia mbili

Mabao mawili yaliyofungwa na winga wa Kimataifa wa Tanzania Saimon Msuva, yameisaidia Difaa Al Jadida inusurike na kipigo kutoka kwa Olympique de Khouribga kwa kulazimisha sare ya mabao 3-3 ugenini.

Matokeo hayo yanaiongezea pointi moja Jadida na kushuka kwa nafasi moja hadi ya nne kwenye Ligi ya Morocco yenye timu 16, ikifikisha pointi zake 38 baada ya kucheza mechi 25.
Msuva alifunga mabao yake dakika za 65 na dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida, hilo likiwa bao lililoinusuru Jadidi kupoteza mechi.

Msuva amekuwa na mafanikio tangu ajiunge na Al Jadida, sasa amefikisha mabao 15.

Timu hiyo imetinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa, Msuva akiwa anashika namba mbili katika wapachika mabao vinara akiwa na mabao manne.