Yanga yatua Ethiopia na matumaini kibao

Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amesema wamejiandaa kikamilifu na watahakikisha wanafuzu hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Keshokutwa Jumatano, April 18 Yanga itaikabili Wolaitta Dicha kwenye mchezo wa marudiano unaopigwa nchini Ethiopia.

Hiyo ni nafasi pekee kwa Yanga ambayo awali ilikuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kutolewa na Township Rollers na kudondokea kwenye michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika.

Mkwasa amesema huo ni mchezo wa kujitathmini na kuwathibitishia mashabiki wao pamoja na Watanzania kuwa waliteleza kwa kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na walitambua makosa yao.

Mkwasa amesema ushindi wa mabao 2-0 waliopata nyumbani umeongeza hamasa ya wachezaji na wameahidi kumaliza kazi nchini Ethiopia

"Tumedhamiria na tutahakikisha tunapata matokeo yatakayotuwezesha kutinga hatua ya makundi"

Mchezo huo utapigwa kwenye mji wa Hawassa yalipo Makao ya klabu ya Wolaitta Dicha, mji ambao upo umbali wa kilomita 275 kutoka mji Mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Kikosi cha Yanga kiliwasili jana nchini Ethiopia tayari kwa mchezo huo utakaorushwa mubashara na runinga ya Azam.