Simba hii ni hatari, yaifumua Prisons 2-0

Vinara wa ligi kuu ya Vodacom, Simba wamezidi kuchanja mbuga kuelekea ubingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya kuilaza Prisons mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja Taifa jijini Dar es salaam.

Simba iliyotawala mchezo huo kwa muda mwingi ikipeleka mashambulizi mengi langoni mwa Prisons, iliandika bao lake la kuongoza kwenye dakika ya 35 mfungaji akiwa nahodha wake John Bocco.

Krosi ya Erasto Nyoni iligonga mwamba wa pembeni kabla ya kukutana na 'ndosi' ya Bocco na mpira kujaa kimiani.

Simba ilikwenda mapumziko ikiongoza kwa bao hilo moja. Prisons ilifanya shambulizi moja pekee kwenye lango la Simba katika kipindi hicho cha kwanza.

Kipindi cha pili Simba iliendeleza kasi iliyomaliza nayo kipindi cha kwanza ambapo ilikosa nafasi mara kadhaa kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji Shiza Kichuya ambaye alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Prisons.

Bao la pili la Simba lilifungwa na Emanuel Okwi kwenye dakika ya 82 kwa mkwaju wa penati baada ya Bocco kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Adhabu hiyo ya penati pia ilipelekea mlinzi wa Prisons El Fadhil kutolewa nje baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Ushindi huo ni habari njema kwa mashabiki wa Simba ambao huenda wakaanza maandalizi ya sherehe za ubingwa mapema kuliko inavyodhaniwa.

Simba imefikisha alama 58 sasa ikiongoza kwa tofauti ya alama 11 dhidi ya Yanga iliyo nafasi ya pili ikiwa na alama 47 huku pia ikiwa na michezo miwili ya kiporo.

Simba pia imefunga mabao 57 ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo msimu huu.

Matokeo ya michezo yote iliyopigwa leo;